Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi inatathminiwa pia kwa kuangalia mwenendo wa biashara ya nje na akiba ya fedha za kigeni. Katika mwaka 2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 48.8 na kufikia nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 2,054.8, kutoka nakisi ya Dola za Kimarekani milioni 4,011.6 kwa mwaka 2015. Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la thamani ya madini hususan dhahabu, bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii, pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za kukuza mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida. Katika kipindi hicho, thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 5.2 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 9,381.6 wakati thamani ya bidhaa na huduma toka nje zilipungua kwa asilimia 13.7 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 10,797.4
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Desemba 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola ya Kimarekani milioni 4,325.6 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.2. Aidha, rasilimali za fedha za kigeni za mabenki ya biashara zilifikia Dola ya Kimarekani milioni 768.2, wakati amana za fedha za kigeni zilizohifadhiwa na wakazi katika benki za biashara zilifikia Dola za Kimarekani milioni 2,870.8. Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha.
Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
Mheshimiwa Spika, kiashiria kingine cha hali ya uchumi ni mwenendo wa sekta ya fedha. Katika kipindi kilichoishia Desemba 2016, tathmini ya hali ya mabenki yetu na taasisi za fedha inaonesha kuwa mabenki yetu ni imara na salama, yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha: Kiwango cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total capital to total risk weighted assets and off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia 17.8 kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 10.0.
Hali ya Ukwasi katika uchumi
Mheshimiwa Spika, ukwasi (liqudity) ni kiasi cha fedha kilichopo katika uchumi na unajumuisha fedha taslim, amana katika mabenki zilizopo Benki Kuu. Utoshelevu wa ukwasi katika uchumi unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali ikiwemo ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi, na upatikanaji wa huduma za kifedha. Pale ambapo imedhihirika kuwa kuna upungufu wa ukwasi katika uchumi, Serikali kupitia Benki Kuu huchukua hatua mbalimbali za kisera kuchochea shughuli za kiuchumi. Hatua hizi ni pamoja na kuongeza ujazi wa fedha na kuboresha mazingira kwa sekta binafsi kukopa. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inaweza kupunguza kodi na kuongeza matumizi ya Serikali.
Hali ilivyo sasa
Mheshimiwa Spika, hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi nchini ni kama ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi (Liquid assets to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 42.4 ukilinganishwa na asilimia 37.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2015 na ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Amana za wateja katika mabenki zilipungua kidogo kutoka shilingi trilioni 20.73 mwezi Desemba 2015 kufikia shilingi trilioni 20.57 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, amana za serikali kwenye mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya amana zote za mabenki. Aidha, jumla ya rasilimali za mabenki zimeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 26,917.2 mwezi Desemba 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 27,978.2 mwezi Desemba 2016, sawa na ongezeko la asilimia 2.6.
Mikopo kwa Sekta Binafsi
Mheshimiwa Spika, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 7.2 katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2016 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 24.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na tahadhari iliyochukuliwa na mabenki kufuatia kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 6.4 Desemba, 2015 hadi asilimia 9.5 Desemba, 2016.
Mheshimiwa Spika, ni vema pia ieleweke kuwa kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya hivi karibuni siyo kwa Tanzania pekee. Kwa mfano, kiwango cha ukuaji wa mikopo kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya kilipungua kutoka asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia asilimia 4.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Aidha, Nchini Uganda mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia 25.2 mwezi Septemba 2015 hadi asilimia -1 mwezi Septemba 2016. Pia mwenendo usioridhisha ulijitokeza katika mikopo chechefu katika nchi hizo jirani na kusababisha baadhi ya mabenki hususan Crane Bank ya Uganda kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wasiofikiwa na mabenki umeendelea kuongezeka kutokana na ubunifu wa mipango ya utoaji wa huduma za malipo ya rejareja kupitia simu za mikononi, pamoja na huduma za uwakala wa mabenki (agent banking services).
Benki zilizopata msukosuko katika robo ya kwanza
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai – Desemba 2016, CRDB na TIB Development Bank zilipata hasara. Hasara ilisababishwa na tengo kwa ajili ya mikopo chechefu (provision for non performing loans). Aidha, Twiga Bancorp imewekwa chini ya uangalizi wa BOT, jambo ambalo si geni. Crane Bank Ltd ya Uganda iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya nchi hiyo Oktoba 2016 kama ilivyokuwa Imperial Bank Kenya, Oktoba 2015. Licha ya hali hiyo, benki nyingi zikiwamo CRDB na TIB Development Bank, zimebaki kuwa na mitaji na ukwasi wa kutosha kwa mujibu wa Sheria. Aidha ni vema kukumbuka kwamba jumla ya benki na taasisi za fedha nchini kote ni 66 na zina matawi 783. Hivyo, kwa benki tatu (3) tu kupata msukosuko katika robo moja ya mwaka si sababu ya kuzua taharuki. Ikumbukwe pia kuwa hiki ni kipindi cha mpito na taasisi nyingi za Kibenki zilikuwa zinafanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya kuyataka Mashirika na Taasisi za umma kufungua akaunti za mapato BOT na kuhamishia amana za taasisi hizo hususan akiba za muda maalum (fixed deposit) kutoka kwenye mabenki ya biashara. Matarajio ya Serikali ni kuwa mara utaratibu mpya utakapozoeleka shughuli za kiuchumi zitaendelea katika uhalisia wake na Benki zitaendelea na huduma za mikopo na hivyo kuongeza ukwasi katika Uchumi.
Uamuzi wa Serikali Kuzitaka Taasisi za Umma Kufungua Akaunti za Mapato Benki Kuu kama sababu ya Kupungua kwa Ukwasi katika uchumi.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Waheshimiwa Wabunge na jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu na amana za muda maalum. Akaunti za matumizi bado ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo kupitia akaunti hizo. Hivyo, bado benki za biashara ni kiungo muhimu kati ya mashirika ya umma na watoa huduma kwa mashirika hayo. Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukuma benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha hadi vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa (corporate sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati fungani za Serikali. Uamuzi huu umesaidia katika usimamizi wa mapato na matumizi ya Mashirika hayo na pia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha kupitia Benki Kuu. Aidha, Serikali imeacha kukopa fedha zake yenyewe na kwa gharama kubwa. Kwa kuwa amana za Serikali kwenye mabenki ya biashara ni sehemu ndogo tu (asilimia 3) ya amana zote za mabenki, madai kwamba uamuzi wa Serikali kuondoa fedha za mashirika na taasisi kwenda kwenye akaunti za mapato BOT umesababisha kupungua kwa ukwasi hayana uzito.
Mheshimiwa Spika, naomba kusisistiza kuwa uamuzi wa Serikali kuzitaka taasisi za umma kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu utaendelea kubaki kama ulivyo. Kwa kifupi, fedha hizi za umma zilikuwa zinatumika vibaya na mashirika lakini pia zilitumika kuikopesha Serikali fedha zake yenyewe kwa riba kubwa kupitia biashara ya dhamana na hati fungani za Serikali. Kasoro hiyo iliondoa motisha kwa mabenki ya biashara kupeleka huduma za kifedha vijijini na hata kukopesha sekta binafsi (crowding out credit to the private sector).
Utoaji wa fedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2016
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kupeleka fedha katika Halmashauri zetu kwa kuwa ndiko utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi unapofanyika. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016/17, Serikali ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 114.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo. Aidha, katika robo ya pili ya mwaka, Serikali iliongeza mgao wa fedha zilizoenda kwenye Halmashauri ambapo kiasi cha shilingi bilioni 203.4 zilipelekwa. Serikali itaendelea kupeleka fedha katika halmashauri kwa kipindi kilichobaki kulingana na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za halmashauri za kuwahudumia wananchi.
Ulipaji wa Madai Mbalimbali
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni 30, 2016 kiasi cha shilingi bilioni 3, 113.7 ziliwasilishwa ikiwa ni madai ya wakandarasi, watumishi, wazabuni na watoa huduma. Baada ya Serikali kufanya uhakiki kupitia kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa madai halali yalikuwa shilingi bilioni 2,934.2 na madai yaliyokosa vielelezo na hivyo kukosa uhalali yalikuwa shilingi bilioni 179.5.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha nusu mwaka wa 2016/17, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 600.2. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 42.35 zilikuwa ni kwa ajili ya madai ya watumishi, shilingi bilioni 49.46 kwa ajili ya wazabuni, shilingi bilioni 11.2 kwa ajili ya watoa huduma, shilingi bilioni 30.0 kwa ajili ya madai ya vyombo vya ulinzi na usalama, na shilingi bilioni 467.2 kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali ikijumuisha shilingi shilingi bilioni 2.0 kwa ajili ya makandarasi wa maghala na skimu za maji.
Mheshimiwa Spika, kuhusu madeni ya pembejeo, Serikali bado inaendelea na uhakiki wa madeni hayo ili kubaini madai halali na yasiyo halali. Hata hivyo, katika kipindi cha Julai – Desemba, 2016 Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 10.0 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Aidha, katika kuhakikisha madai ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma wa ndani wanapewa kipaumbele, Serikali imeweka mkakati wa kutenga fedha kila mwezi ambapo mwezi Januari 2017 Serikali imetenga jumla shilingi bilioni 70.0.
Jedwali Na. 2: Madeni yaliyolipwa kwa kipindi cha Julai - Desemba, 2016
Jedwali Na. 3: Deni lililobaki baada ya malipo ya hadi Desemba 2016
Mwenendo wa Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa linajumuisha mikopo ambayo hukopwa na Serikali kutoka nje na ndani ya nchi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kujaza nakisi ya bajeti. Deni la nje hukopwa kutoka kwenye taasisi za kifedha kama vile Benki ya Dunia, nchi Wahisani na pia kutoka kwenye benki za biashara wakati deni la ndani linapatikana kwa kuuzwa kwa dhamana za Serikali (treasury bills) na hatifungani (Treasury bonds), mikopo kutoka Benki Kuu ya Tanzania na benki za biashara za ndani.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134. Aidha, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linasimamiwa kikamilifu Serikali inakamilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 ili kuimarisha usimamizi wa Deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Desemba, 2016, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje lilifikia Dola za Kimarekani milioni 19,021.9 (debt stock) ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 18,459.3 Juni, 2016 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 3.05. Kiasi hiki cha deni hakijumuishi deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii linalokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,725.8 ingawaje deni hilo limezingatiwa katika tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, ongezeko la deni hilo limetokana na mikopo iliyopo na mipya iliyopokelewa na Serikali na ambayo bado haijaiva kutoka mikopo ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile reli ya Tazara, daraja la Kikwete mto - Malagarasi, barabara ya Morogoro – Dodoma, barabara ya Dodoma – Singida – Arusha, barabara ya Mwanza – Bukoba, mradi wa Maji ziwa Victoria, Bomba la Gesi Mtwara – Dar es Salaam, barabara ya Dodoma - Singida – Mwanza, miradi ya umeme Kinyerezi I & II, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano n.k. Miradi ambayo iligharamiwa na mikopo hiyo imeelezewa kwa kina katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 na katika kitabu cha Uchambuzi wa Deni la Taifa pamoja na miradi inayofadhiliwa na deni hilo. Pamoja na miradi iliyotajwa, naomba kuweka mezani taarifa ya Agosti,2016 ya uchambuzi wa Deni la Taifa na miradi yote iliyofadhiliwa na deni hilo tangu uhuru.
Ulipaji wa Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika, ulipaji wa Deni la Taifa hauangalii ukubwa wa deni lililopo (stock of debt) bali kadri deni linavyoiva (debt maturity). Hali ilivyo sasa sehemu kubwa ya Deni la Taifa linaiva kwa kipindi cha muda mrefu (long term maturity). Kutokana na hali hiyo, kwa wastani (average time to maturity) wa deni lililopo sasa litaiva katika kipindi cha miaka isiyopungua 11.9. Hali hii inaashiria kwamba athari zake kwenye bajeti ziko chini (low refinance risk).
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa madeni ya nje na ndani kwa mujibu wa mikataba. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016 Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni shilingi bilioni 1,822.3 na deni la nje ni shilingi bilioni 747.8. Malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji (rollover) ya shilingi bilioni 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi bilioni 455.2
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuendelea kulipa kwa wakati mikopo yote ya nje inayoiva kwa mujibu wa mikataba. Aidha, Serikali itaendelea na utaratibu wa kukopa kwa ajili ya kulipa mtaji kwa amana zinazoiva (rollover of principal maturities of T-bonds and T-bills). Lengo la kuendelea na utaratibu huo (rollover) ni kutoa ahueni kwenye bajeti ya kila mwaka husika na ni utaratibu wa kawaida unaotumika na nchi nyingi duniani.