Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Wizara ya Fedha ina jukumu la kukokotoa Pato la Taifa kwa robo
Mwaka ili kuwapatia takwimu kwa wakati,
wadau wa takwimu za Pato la Taifa katika vipindi vifupi vya robo mwaka ili
kuweza kutathmini mabadiliko ya ukuaji wa uchumi.
Ukuaji
halisi wa Pato la Taifa la Tanzania kwa bei za soko uliongezeka kwa kasi ya
asilimia 6.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na
kasi ya asilimia 6.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jumla ya thamani ya
Pato la Taifa katika kipindi husika ilikuwa Shilingi 5,012,935 milioni mwaka
2013 ikilinganishwa na Shilingi 4,699,884 milioni mwaka 2012.
Shughuli za
kiuchumi za kilimo zilifikia kasi ya ukuaji ya asilimia 5.3 katika kipindi cha
robo ya pili ya mwaka 2013 zikilinganishwa na asilimia 5.1 ya robo kama hiyo
mwaka 2012. Katika kipindi hicho, kulikuwa na mvua za kutosha katika mikoa inayozalisha
mazao kwa wingi. Aidha, maelekezo ya ma-ofisa Ugani kwa wakulima kama kuchagua aina bora ya mbegu yalisaidia kuongeza
uzalishaji.
Shughuli za
uvuvi zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 2.4 katika robo ya pili ya mwaka
2013 ikilinganishwa na asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kasi ya
ukuaji huu ilipugua kutokana na kupungua kwa mavuno ya samaki kutoka kwenye
maziwa, mito na mabwawa.
Shughuli za Uchumi za Viwanda
na Ujenzi
Shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto ziliongezeka
kwa kasi ya asilimia 4.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa
na kuporomoka kwa kasi ya ukuaji wa asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho
mwaka 2012. Kuongezeka kwa kasi hii ya ukuaji ilitokana na kuongezeka kwa
uzalishaji wa madini ya almasi na Tanzanite katika robo ya pili ya mwaka 2013.
Shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilifikia kasi ya
ukuaji ya asilimia 5.8 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa
na kasi ya asilimia 8.2 mwaka 2012. Kupungua kwa kasi ya ukuaji ya asilimia 2.4
(percentage point) kulitokana na kupungua kwa uzalishaji wa sementi, vyakula
vilivyosindikwa na nguo.
Uzalishaji wa nishati ya umeme ulifikia kasi ya ukuaji wa
asilimia 4.5 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kuporomoka
kwa kasi ya ukuaji ya asilimia 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kuongezeka
kwa ukuaji wa nishati ya umeme kwa asilimia 5.6 (percentage point) kulitokana na
kuongezeka kwa uzalishaji wa nishati ya umeme unaotokana na mafuta na gesi.
Ukuaji
wa Shughuli za Uchumi za Utoaji Huduma
Shughuli za biashara za jumla na reja reja, ukarabati wa
magari na pikipiki na vifaa vingine vya majumbani zilifikia kasi ya ukuaji wa
asilimia 5.9 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na
kasi ya asilimia 7.0 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2012. Kupungua
kwa kasi kwa asilimia 1.1 (percentage point) kulitokana na kupungua kwa bidhaa
zilizotengenezwa hapa nchini na zilizoagizwa kutoka nje ya nchi zilizouzwa katika
kipindi hicho. Shughuli za upangishaji
nyumba, na shughuli zingine za biashara zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 6.7.
Shughuli za uchukuzi na mawasiliano zilifikia kasi ya
ukuaji wa asilimia 14.8 katika kipindi husika. Shughuli nyingine ni huduma za
Hoteli na migahawa zilizofikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.2; Shughuli za
uendeshaji Serikali zilifikia kasi ya asilimia 5.0, Elimu asilimia 5.7 na
huduma za Afya na shughuli nyinginezo zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.8 katika
kipindi hicho.
Imetolewa na:
Morrice Oyuke
Mkurugenzi wa Takwimu za Kiuchumi
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dar es Salaam
Kwa
mawasiliano zaidi kuhusu Takwimu za Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka
2013, wasiliana na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu kwenye anuani zifuatazo:
Mkurugenzi Mkuu,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
S.L.P. 796, Dar es Salaam.
Simu: +255 22 212 2722/3/4
Nukushi: +255 22 2130852
0 comments:
Post a Comment