Sunday, December 23, 2012

KAMPUNI ZA NDEGE ZINAZOTOA HUDUMA KUPITIA M-PESA ZAONGEZEKA


DAR ES SALAAM, Tanzania
Idadi ya Kampuni na Mashirika ya ndege nchini ambayo yameingia kwenye mkataba na Vodacom katika kuwawezesha wateja wake kulipia tiketi za usafiri huo kupitia M-Pesa imeongezeka.

Hadi kufikia sasa Kampuni zilizoingizwa moja kwa moja kwenye mfumo wa huduma hiyo ni pamoja na Shirika la Ndege la Precision, Coastal Travels, Auric Air na Skylink Tanzania. Huku Kampuni nyingine zikipatikana kwenye orodha kwa kuingiza namba ya biashara ya kampuni husika.

Ili kufanya malipo mteja atatakiwa kupiga namba *150*00# na kuchagua malipo ya bili kupitia orodha ya M-pesa na kuingiza namba ya biashara ya Shirika au Kampuni husika ikifuatiwa na namba ya malipo na kiasi cha fedha itakayolipwa.

Mkuu wa Kitengo cha Udhamini na Mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twissa, amesema kuwa njia hiyo ni ya haraka, rahisi na itaokoa muda kwa wateja, hususan katika msimu huu wa sikukuu za Krismass na Mwaka mpya, ambapo wateja wengi hupendelea kusafiri.

Amesema Vodacom inaona fahari kuingia katika ushirikiano huu na wabia wake, kwani kwa kufanya hivyo huduma husika itasaidia kuondoa foleni na misongamano ambayo ni dhahiri inapoteza muda wakati wa ukataji tiketi.

Aidha ameeleza faida za huduma hiyo kuwa ni pamoja na kukata tiketi ukiwa popote, pia hakuna sababu ya kutembea na fedha taslimu, hatua inayomhakikishia usalama mteja, na pia mteja akikata tiketi papo hapo atapata salio la bure la muda wa maongezi wa shilingi 1000.

Aidha, Twissa anaeleza kuwa ushirikiano huo utatoa njia mbadala katika malipo ya tiketi, na kusisitiza kuwa huduma ya M- pesa ni salama, haraka na ya uhakika, kwa kuwa imeleta mapinduzi katika huduma mbalimbali za kifedha tangu kuanzishwa kwake miaka minne iliyopita.

"Tunaamini kuwa tutaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wetu. Tunajivunia ushirikiano huu na tunatarajia utakuwa na mafanikio makubwa katika kukidhi mahitaji ya huduma kwa wateja wetu," anasema Twissa.

Huduma ya M-Pesa ya Vodacom Tanzania ina mawakala zaidi ya elfu 20,000 nchini kote, na ni pekee ambayo inaongoza, kwa usalama na ubora katika kukidhi mahitaji ya huduma za kifedha kwa Watanzania walio wengi.

0 comments:

Post a Comment