Sunday, December 9, 2012

TRENI YA ABIRIA YAREJESHA SAFARI ZAKE MWANZA TANGU MWAKA 2009

Treni ikiwasili Jijini Mwanza leo

MWANZA, TANZANIA
MAMIA ya wakazi wa jiji la Mwanza, leo walilipuka kwa shangwe na vigelegele wakati wakiilaki Treni ya Abiria iliyowasili hapa kwa mara ya kwanza baada ya kusitishwa kwa safari zake toka Disemba 2009.

Treni hiyo iliwasili katika Stesheni ya mjini Mwanza saa 5:55 mchana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba akiwa ni mmoja wa abiria waliopokewa na wananchi hao walioongozwa na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga.

Huku baadhi wakiwa na mabango yaliyobeba ujumbe mbalimbali wa kuipongeza Serikali na Waziri wa Uchukuzi Dk Halson Mwakyembe, wananchi hao walianza kushangilia mara tu Treni hiyo ilipotokeza kwenye yadi ya stesheni.

Shangwe hizo zilipokewa na abiria waliokuwemo ambao walionyesha nyuso za furaha na kuwapungia mikono wananchi na viongozi hao wakiwemo ndugu na jamaa waliokuwa wamefika kuwapokea.

“Hayawi hayawi leo yamekuwa, wao wao Treni ya abiria kuja Mwanza” ndivyo baadhi ya wananchi walivyosikika wakiimba wakati Dkt Tizeba akishuka pamoja na abiria wenzake na kupokewa na viongozi wa Chama na Serikali.

Pamoja na Konisaga aliyekuwa akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo, wengine waliipokea Treni hiyo ni pamoja na Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Amina Masenza, Meya wa Jiji la Mwanza Stanslaus Mabula na katibu wa CCM wilayani Nyamagana, Deogratias Rutta.

Baadhi ya abiria wakiwemo Mwaka Hussin mkazi wa Tabora na Moshi Mfalila mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam , wakizungumza na Uhuru walisema kuwa wanaishukuru serikali kurejesha ufasiri huo wa wanyonge.

“Tunaishukuru serikali usafiri huu mzuri, japo viti vya mabehewa naona vimechoka, waviboresha na kudhibiti vibaka wasiingie ovyo.” Alisema Hussein huku Mfalila akidai kuwa waboreshe Injini za usafiri huo ili abiria wasikwame tene kama walivyokwama juzi kwa saa nne, Ubungo.

Wakazi wa jiji la Mwanza waliofika kuilaki Treni hiyo, wakiwemo Sikitu Chibulule, Nelson Wilson na Mwanaidi Rajabu, walimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ya kufufu usafiri wa Reli na kusema kuwa serikali ya CCM sasa inafurahisha kwa uchapa kazi.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL nchini, Kipallo Kisamfu alisema kuwa, shirika lake lina furaha isiyo kifani kuwasili kwa Treni hiyo Mwanza, siku ambayo ina historia ya miaka 51 Uhuru wa Tanzania Bara.

“Disemba 2009 niyo ilikuwa mara ya mwisho Treni hii kuja Mwanza safari zake zikasitishwa, lengo letu ni kurudisha ufanisi wa Treni uliokuwepo awali, lengo hilo si jepesi ni zito lakini kwa hali tuliyofikia tutafika huu ni mwanzo tu wa jitihada za serikali yetu.” Alisema Kisamfu.

Alieleza kuwa mpango wa serikali ni kuhakikisha Treni inafufuka na kutoa mchango wake mkubwa katika huduma za jamii na kukuza pato la taifa, hivyo pamoja na kuanza na mabehewa machache, huduma hiyo itaboreka siku hadi siku kwani ukarabati wa mabehewa mengine na vichwa vya Treni, unendelea.

0 comments:

Post a Comment