Saturday, June 22, 2013

MFUKO WA MAMA ANNA MKAPA KUWAFUNDA WAJASRIAMALI

MAMA ANNA MKAPA
Na Magreth Kinabo,Maelezo
JUMLA ya wajasiriamali wapatao 250 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani watapatiwa mafunzo ya  elimu ya ujasiriamali, uzalishaji bora  wa bidhaa na uundaji wa vikundi vya uzalishaji ili kukidhi oda kulingana na mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo ya muda wa siku tatu kuanzia Juni 25, mwaka huu yatafunguliwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Abdallah Kigoda saa tatu asubuhi  katika ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani jijini Dares Salaam ambapo yatasaidia kukabiliana na changamoto juu  ya masuala hayo.

Hayo yalisemwa na  Mkurugenzi  Mtendaji wa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa wote(EOTF),  Stephen Emmanuel  kutipia taarifa yake aliyoitoa leo kwa vyombo vya habari, ambapo alisema mafunzo hayo  yanafadhiliwa na mfuko huo unaosimamiwa na  Mke wa Rais  wa Awamu ya  Tatu ,Mama Anna Mkapa.

“ Elimu  inayotolewa  inawezesha wanawake wajasiriamali ambao ndio wazalishaji wakuu wa bidhaa za kilimo,ufugaji, sanaa za mikono n.k. kufanya biashara endelevu  na kujikomboa kiuchumi, kuondoa ujinga na maradhi katika jamii yetu ya Tanzania  - KUPIGA VITA UMASIKINI,” alisema Emmanuel.

Alisema katika mafunzo hayo kutakuwepo na mada za fursa na changamoto za wanawake hao katika biashara, huduma kwa mteja, umuhimu wa viwango vya bidhaa(TBS), Bar Code, stadi za masoko, fursa za  mitaji kutoka taasisi za fedha.
Mada nyingine ni, ubadilishaji ujuzi, haki za wanawake, rasimu ya katiba mpya na kuhamasisha mapambano ya maradhi  hatarishi ya saratani ya matiti na uzazi, malaria na ukimwi  yanayomaliza nguvu kazi ya taifa.

Aliongeza kuwa  mada hizo zitatanguliwa na mchango wa msanii maarufu Judith Wambura “Lady  Jay De” kuwahamasisha  wanawake kutumia vipaji vyao kujikomboa katika wimbi la umasikini na kujitegemea. Pia atakuwepo mkongwe wa mashairi  ajulikanaye kwa jina la Tambalizeni ambaye atatoa ngonjera juu ya  uwezeshaji wa wanawake hao kupitia mfuko huo.

Tangu mfuko huo uanzishwe mwaka 1997 umeshatoa mafunzo  hayo kwa wanawake hao 3,650, ambapo asilimia 85 wanatoka vijijini, pia wanapewa fursa ya kushiriki katika maonesho ya   sabasaba na nje ya nchi.

Aidha aliongeza kuwa mpaka sasa EOTF imewezesha wanawake hao  zaidi ya 2500 kushiriki kwenye maonesho  hayo na nje ya nchi . Hivyo mauzo na oda walizopata katika  maonesho  ya 36 ya sabasaba  ya mwaka 2012 , yalifikia  sh. milioni 55.9.

0 comments:

Post a Comment